Translate

Jumapili, 5 Aprili 2015

Historia ya Jiko banifu/Sanifu KCJ

Historia ya jiko sanifu barani Afrika inaanzia miaka ya 1970 na kuendelea mpaka miaka ya 1980.Tokea mwaka 1982 Shirika la Nishati na Mazingira Kenya KENGO lilifanya tafiti ikishirikiana na wataalamu wasomi mmojawapo ni Dr Maxwell Kinyanjui kufanya tafiti na kuendeleza matumizi ya jiko la ufinyanzi.Jiko hili lina chimbuko kutoka Thailand ambako lilianzia kutokana na jiko ‘ndoo’.Taasisi kama CARE,UNICEF na Bellerive zimefanya kazi kubwa kutoa mchango wa kifedha na kuwezesha kuendeleza jiko na namna ya kulitengeneza pamoja na mashirika ya misaada kama Marekani (USAID),Ujerumani (GTZ) na mashirika mengineyo. Mtaalamu,msanifu na msomi Dr Maxwell Miringu Kinyanjui kutoka Kenya  alifanikisha maendeleo ya jiko hili kuwa sanifu  na bora kwa matumizi ya nishati ndogo ya mkaa.Kutokana na tafiti,fafanuzi na biashsra ikafanya jiko sanifu  (ufinyanzi) kutambulika kama jiko la kupunguza matumizi  ya nishati ya kupikia mkaa Kenya.Kwa mara ya kwanza jiko kwenda sokoni lilikuwa linauzwa bei ghali kutokana na watumiaji wengi baadhi yao kuwa ni maskini wanaotumia jiko la mafiga matatu. Baada ya kufikiriwa kwa makini hitimisho lilifikiwa na wataalamu kwamba kutokana na jiko ni geni sokoni basi lisi wekewe ruzuku ili liende sokoni lishindane kama bidhaa nyingine na kuleta ushindani thabiti. Mwanzo jiko Sanifu (ufinyanzi) lilikuwa ghali,mauzo yalikuwa taratibu na ubora ulitofautiana kutokana na kuigwa utengenezaji na wasanifu wengine bila kufuata vigezo kuwa na majiko sanifu feki yasiyo na ubora kama ulio kusudiwa.Kuendelea  kuongezeka kwa watengenezaji na wauzaji wa majiko sanifu kukaongeza ushindani na hii ikaongeza uvumbuzi wa kutengeneza chaga za jiko kwa kutumia udongo ufinyanzi pamoja na simenti ili kupata chaga bora itakayo akisi joto na kukaa nalo muda mrefu.

Sehemu ya jiko

Jiko sanifu au jiko banifu lina  chaga ambayo ndio inayobeba mkaa wa moto na kuhifadhi  kutunza kwenye chaga amabayo imetengenezwa kwa udongo wa ufinyanzi ulio na uwezo wakuhifadhi  joto. Hivi sasa  chaga zinaboreshwa kwa  udongo ufinyanzi unachanganywa na simenti  kufanya chaga iwe ngumu na isiharibike mapema.Baadhi ya wasanifu na mafundi majiko wanaoiga jiko hili wamekuwa wakitengeneza chaga zisizo na ubora ulio kusudiwa. Baadhi ya watengenezaji wa majiko haya barani Afrika kama Cookswell Jiko Kenya na Tatedo Tanzania wanashauri chaga  bora ni zile zenye kudumu mda mrefu na uwezo wa kuhifadhi joto lisipotee kuonyesha uendelevu. Jiko hili Sanifu limechangia kukua ujasiriamali  kwa  watengenezaji wa majiko ya kawaida ya bati sasa hivi wanatengeneza  fremu ya jiko na chagga baada ya jiko hili kuwa maarufu katika kaya za Afrika Mashariki.

Kusambaa kuingia Tanzania

Jiko hili sanifu liliingia Tanzania miaka ya 1990 kutokea Kenya pale Shirika la Nishati Asili na Jadidifu Tanzania TATEDO kupata mafunzo kutoka kwa msanifu na muendelezaji  jiko hili barani Afrika Dr Maxwell Kinyanjui. Tatedo walikuwa wa kwanza  kueneza matumizi ya jiko hili na kuwezesha wajasiriamali wa nishati jadidifu ili kutumia jiko hili katika kaya za Tanzania.Mtaalamu wa Cookswell Jiko  Teddy Kinyanjui  anasema ili bidhaa ya jiko sanifu iweze kupenya sokoni inahitaji miaka 10 mpaka 20.Kwa hiyo kwa jiko sanifu (ufinyanzi) KCJ mpaka kufikia mwaka 2002 jiko sanifu lilikuwa limepenya soko la Tanzania na mpaka kufikia mwaka 2012 jiko hili lilikuwa linajulikana na maarufu kama jiko banifu,bora au sanifu. TATEDO wameendelea kupanua aina ya bidhaa hii ya jiko sanifu kwa kutengeneza aina mbalimabali za jiko hili kukidhi  mahitaji ya wateja mbali mbali kama Sazawa.

Faida ya Jiko sanifu

Yana punguza matumizi ya kichochezi nishati (mkaa) kwa asilimi sabini na moja 71%.
Hayachochei  uzalishaji wa moshi hewa ukaa (carbon).
Yana usalama wa joto na bati kutokana na joto kuhifadhiwa katika chaga bila kutorokea kwenye bati
Kumeongeza ajira kwa watengenezaji na ujasiriamali kwa viwanda vidogo vya kutengeneza chaga za ufinyanzi
Yanahifadhi nishati kwenye chaga
Yana dumu muda mrefu
Uzoefu unaonyesha yanapunguza gharama ya matumizi ya mkaa kwa asilimia hamsini 50%
Jiko Sanifu na Mkaa
Jiko hili linategemea mkaa unaotokana na mti ili kuchochea na kuhifadhi joto kwa matumizi ya kupikia.Kumekuwa na dhana potofu kwamba mkaa unatumika na maskini tu na hauna faida yoyote katika jamii au ni ‘nuksi’ katika uhifadhi wa misitu ya asili.Inashauriwa kupanda miti ilikuendelea kupata bidhaa ya mkaa inyotumika katika majiko banifu.Mkaa ni nishati jadidifu kama miti itakuwa inapandwa kwa ajili ya bidhaa mkaa.Pia kila mwananchi kupanda mti katika eneo lake analoishi ili kutengeneza mkaa wake mwenyewe (DIY) kwa kukabonisha  matawi ya miti,magunzi mapute ya nazi na kupata mkaa rafiki mazingira (eco charcoal).

 







Imeandikwa na Mckene Ngoroma kwa msaada wa vyanzo vya taarifa Teddy Kinyanjui  wa  COOKSWELL  JIKO KENYA na TATEDO Tanzania


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni